FUTA MACHOZI MPENZI-14
NYEMO CHILONGANI
“Mambo mrembo,” ilisikika sauti kutoka kwa jamaa aliyesimama pembeni, mkononi alikuwa akikiendesha chombo cha kuwekea bidhaa mbalimbali.
“Safi!” aliitikia Melania.
“Umependeza,” alisema mwanaume huyo lakini Melania hakujibu kitu, alinyamaza, akamwangalia mwanaume huyo na kuendelea na shughuli zake.
Mwanaume huyo aliyejitambulisha kwa jina la Godson Mabula hakuacha kumwongelesha Melania, muda mwingi alikuwa akimzungumzisha lakini msichana huyo hakumpa ushirikiano wowote ule.
Alitokea kumpenda, msichana huyo alikuwa mzuri wa sura, kila alipomwangalia Godson hakutaka kumuacha, kwake, aliwahi kuona wanawake wengi lakini kwa Melania, alionekana kuwa na uzuri wa ajabu.
Godson hakuacha, hakunyamaza, muda mwingi aliendelea kumsemesha msichana huyo ambaye alionekana kutokuwa na muda naye. Waliendelea kuwa ndani ya supamaketi mpaka pale Melania alipoamua kuondoka, Godson hakutaka kubaki, naye akatoka na kuanza kumfuata msichana huyo.
“Melania...” alijikuta akiita. Msichana huyo akageuka na kumwangalia.
“Unasemaje?” aliuliza msichana huyo huku akionekana kuwa na hasira.
“Punguza hasira, hunifahamu, huwezi kumchukia mtu usiyemfahamu dada’ngu,” alisema Godson kwa sauti ya upole iliyoonyesha unyenyekevu wa hali ya juu.
“Una shida gani?”
“Ningependa kuzunguza na wewe.”
“Zungumza nakusikia!”
“Mmh!”
“Zungumza basi unanichelewesha,” alisema Melania huku akionekana kuwa na hasira.
“Samahani! Nahisi si muda sahihi! Naomba unitafute kwenye namba hii!” alisema Godson huku akimpa kikaratasi Melania.
“Nikutafute?”
“Ndiyo! Ila ukipata muda, usipopata muda, acha, usinitafute,” alisema Godson, Melania hakukichukua kikaratasi kile, alichokifanya ni kuufungua mlango wa gari lake na kuingia tayari kwa kuondoka, hata kabla hajafunga vioo vya gari, harakaharaka Godson akamfuata na kumtupia kikaratasi kile ndani ya gari.
“Nitafurahi ukinitafuta,” alisema Godson, akaondoka mahali hapo.
Melania hakuwa na furaha, moyo wake ulikuwa na huzuni tele, mawazo yalikisumbua kichwa chake, kwa muda mwingi sana alikuwa akiwasiliana na William na kumwambia alivyokuwa akimpenda, alivyomtaka awe mpenzi wake lakini mwanaume huyo hakukubali kuwa naye.
Hilo lilimpa mawazo, moyo wake uligota kwa mwanaume huyo, hakuwa na habari ya mtu yeyote zaidi ya huyo. Hakuwa na sura nzuri, alikuwa mbaya lakini moyo wake haukuangalia hilo, kwake, alionekana kuwa mwanaume mwenye sura nzuri kuliko wote katika dunia hii.
“Melania! Tafuta mwingine, kwangu, hapana! Sitokuweza,” alisema William kwenye simu.
“Ila ninakupenda, sijali jinsi ulivyo, ninakupenda William,” alisema msichana huyo.
“Hapana! Tubaki kuwa marafiki. Melania, tukiwa marafiki nitakuwa msaada mkubwa sana katika maisha yako, naomba tuendelee kuwa marafiki,” alisema William.
Hakubadilisha uamuzi wake, aliendelea kumwambia msichana huyo kwamba huo ulikuwa muda wa kuwa marafiki. Alijua kwamba aliumia moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi kwa sababu hakuona kama alikuwa na sababu ya kuwa na msichana huyo mrembo, alimpenda sana Melania lakini alitakiwa kuwa na mwanaume bora hata zaidi ya alivyokuwa.
Hicho kilikuwa kipindi cha kulia, hakunyamaza, wakati mwingine alikuwa akimlaumu Mungu kwa hatua aliyochukua ya kumuonyeshea mwanaume huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa akiutesa moyo wake kupita kawaida.
Siku zikakatika, hata alipokutana na Godson, bado alikuwa na mawazo tele, hakuona kama kulikuwa na mwanaume aliyetakiwa kuuchukua moyo wake zaidi ya William ambaye wala hakuwa na muda naye.
Hakutaka mapenzi ya mwanaume yeyote yule zaidi ya William. Kila siku alikuwa akimfikiria, muda ulisonga mbele, baada ya miezi miwili kukatika, akakata tamaa ya kuwa na William hivyo kuanza kumfikiria Godson.
Hakujua kama mwanaume huyo alikuwa na mapenzi ya dhati au la, alichokifanya ni kulifuata gari lake na kisha kuanza kukitafuta kikaratasi kile, alipokipata, akakichukua na kuanza kuzipiga namba hizo.
“Samahani! Nipo kikaoni, nipigie baada ya nusu saa,” ilisikika sauti ya Godson mara baada ya kupokea simu, hakujua huyo alikuwa nani na alihitaji nini.
Hilo halikuwa tatizo kwa Melania, akavumilia na baada ya nusu saa, akampigia na mwanaume huyo kupokea simu. Kitu cha kwanza kabisa akajitambulisha, Godson akaonekana kusahau kwani kilikuwa kipindi kirefu sana tangu akutane na msichana huyo.
“Melania yupi?” aliuliza.
“Yule wa supamaketi!”
“Ooh! Kumbe wewe mrembo! Umenifanya nisubiri sana kama namsubiri Yesu arudi,” alisema Godson huku akicheka.
“Hahah! Hiyo ndiyo namba yangu!”
“Nashukuru! Kuna masharti ya kupiga?”
“Wala hakuna! Muda wowote ule, ila nisipopokea, jua nipo bize au nimelala!” alisema Melania.
“Basi sawa! Nitakuwa nakubipubipu mrembo!”
“Hahaha! Sawa! Nitakapokuwa na muda wa maongezi nitakuwa nakupigia.”
“Nitashukuru sana!”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa uhusiano wao, wakaanza kuwasiliana kwenye simu, walikuwa kama marafiki, walizungumza kama marafiki lakini kila mmoja alijua ni kitu gani kingekwenda kutokea hapo baadaye.
Baada ya wiki moja tu, Godson hakutaka kubaki kimya, hakutaka kumuona Melania kama rafiki yake hivyo alichokifanya ni kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda kuliko msichana yeyote yule. Melania hakuwa na ujanja, akakubaliana naye na hivyo kuanza uhusiano wa kimapenzi.
Wakawa pamoja, mara kwa mara walikuwa wakionana, Godson ndiye alikuwa mwanaume wa kwanza kulala na Melania, akautoa usichana wake kitu kilichoufanya uhusiano huo kushamiri kupita kawaida.
Wakatambulishana kwamba walikuwa wapenzi, wazazi wa pande zote mbili wakafurahia kile kilichokuwa kimetokea. Siku zikaendelea kukatika zaidi na zaidi na hatimaye Godson akamwambia Melania kwamba huo ulikuwa wakati wa kumvisha pete ya uchumba mbele ya wazazi wake.
Hilo halikuwa tatizo, kitu cha kwanza alichokifanya Melania kabla ya kuwaambia wazazi wake alimwambia William, ilikuwa furaha kwa mwanaume huyo, akampongeza na kumpa hongera kemkem, baada ya hapo ndipo akawaambia wazazi wake.
“Ni lazima tuandae sherehe ndogo nyumbani!” alisema mama yake, Bi Pamela.
“Bila shaka mama!”
“Basi waambie wazazi wake waje, ili atakapofika, akutane na wazazi wake ndani ya nyumba,” alisema mama yake Bi Pamela.
Wakawasaliana na wazazi wa Godson na kuwaambia kile kilichotarajiwa kufanyika usiku huo, haraka sana wazazi hao wakafika nyumbani hao kama njia mojawapo ya kumfanyia sapraizi mtoto wao.
Baada ya saa moja, Godson akampigia simu Melania na kumwambia kwamba alikuwa njiani, hivyo alitakiwa kusubiri.
“Haina shida! Umekumbuka pete?” aliuliza Melania.
“Nimekumbuka!”
“Na wazazi wako umewaambia?”
“Hapana! Nitataka niwafanyie sapraizi na wao, baada ya hapo nitakuchukua na kukupeleka nyumbani, napenda sana kuishi kwenye sapraizi,” alisema Godson, kama kawaida yake akaanza kucheka kicheko cha chini.
Melania akawa na furaha tele, moyo wake ukawa na kimuemue cha kutaka kumuona mpenzi wake. Aliandaa sehemu zote kama ilivyotakiwa, mapambo mazuri na vitu vingi vya kupendezesha nyumba vilikuwa vimewekwa tayari.
Muda ulisonga mbele, dakika zilisogea, sehemu alipokuwa haikuwa rahisi kutumia muda mwingi kama nusu saa lakini kilichowashangaza, dakika arobaini na tano zilipita pasipo mwanaume huyo kuonekana mahali hapo.
Hilo likamtia hofu Melania, harakaharaka akachukua simu yake na kumpigia Godson, simu ilikuwa ikiita lakini haikuwa ikipokelewa. Hilo lilimchanganya, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Hakuacha, aliendelea kumpigia zaidi na zaidi lakini matokeo yalikuwa yaleyale kwamba simu haikupokelewa. Moyo wake ukaanza kujawa na hofu kubwa, akaanza kuogopa na kuhisi kwamba kulikuwa na tatizo, akampigia tena huku akijiahidi kwamba ndiyo ilikuwa mara ya mwisho, muda huo, simu ikapokelewa.
“Godson mpenzi....” alisema Melania huku akianza kutokwa na machozi ya furaha kwani hatimaye mpenzi wake alipokea simu.
“Halo dada!” alisikika mtu mwingine kwenye simu, Melania akashtuka.
“Halo!”
“Wewe ni ndugu yake huyu marehemu?” lilisikika swali kutoka upande wa pili.
“Unasemaje?” aliuliza Melania huku akiwa ameshtuka kupita kiasi, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kumtoka mfululizo.
“Kuna ajali mbaya imetokea hapa Sinza Makab...” ilisikika sauti ya upande wa pili, hata kabla hajamaliza sentensi hiyo, simu Melania akadondoka chini na kupoteza fahamu.
****
William akawa na furaha mno, hakutegemea kama alikuwa akienda kuwa baba. Kila alipokaa, alishindwa kulificha tabasamu lake pana. Hakutaka kumuona Linda akikaa mbali naye, alichokifanya ni kumuhamisha na kuanza kukaa naye katika chumba alichokuwa akikaa chuoni hapo.
Walikuwa kama mume na mke kwa jinsi walivyokuwa wakipendana. Humo, uhusiano wao uliendelea kusonga mbele, watu wakapenda kuwa karibu naye na mpaka siku ambayo alitangaza kwamba kulikuwa na mtandao mpya wa kijamii ambao alitaka kuuzindua, kila mmoja akatamani kuuona.
Taarifa juu ya mtandao huo ikaanza kutangazwa sehemu mbalimbali jijini Massachuesetts nchini Marekani, kila mmoja alitamani kuuona kwani walimwamini William kwamba alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa hivyo hata kuuanzisha mtandao huo ilionekana kabisa kwamba alidhamiria kufanya mapinduzi makubwa.
Maofisa wa mitandao mingine ya kijamii wakakutana katika ofisi zao, walikuwa wakitaka kuangalia namna huo mtandao ulivyokuwa, mioyo yao ilikuwa na hofu kubwa, walionekana kumuogopa William kwani alionekana kuwa mtu hatari sana.
Ndani ya jengo la Ofisi za Facebook, hakukukalika, kila mmoja alikuwa na hofu kwani walijua kwamba William alikuwa mtaalamu mkubwa, mkurugenzi wa mtandao huo, Mark Zuckerberg alikuwa ofisini mwake, alitulia, hakutaka kuonana na mtu yeyote katika kipindi hicho, mbele yake aliona upinzani mkubwa, hakukubali kushindwa, mtandao wake ulikuwa na watumiaji wengi zaidi ya bilioni moja duniani kote, hakutaka kuona akishindwa, ilikuwa ni lazima kupambana.
“Sorry sir,” (samahani mkuu) ilisikika sauti ya dada wa mapokezi ambaye alikuwa ameingia ofisini kwa bosi wake huyo.
“I’m kinda busy, I don’t have time Lisa,” (nipo bize, sina muda Lisa) alisema Zuckerberg.
Hakutaka kuonana na mtu yeyote katika kipindi hicho, alihitaji kutulia na kuuona mtandao huo ambao ulikuwa ukizinduliwa siku hiyo. Alizima simu yake ya mkononi, hakutaka kupigiwa na mtu yeyote yule.
Macho yake yalikuwa kwenye televisheni, alikuwa akimwangalia William alivyokuwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari tena huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
Utulivu haukuwa nchini Marekani tu bali hata sehemu nyingine duniani, kila mmoja alikuwa akifuatilia kile kilichokuwa kikiendelea na kubwa zaidi ni kwamba walitaka kuona jinsi muonekano wa mtandao huo ulivyokuwa.
Ilipofika saa 6:00 mchana, mtandao huo ukaachiwa hewani na watu kuanza kuingiza URL (Uniform Resource Locator) ya mtandao huo na kuanza kuuangalia. Watu wote wakakimbilia kompyuta zao na kuuangalia, ulikuwa ni MeChat, mtandao uliokuwa na muonekano mzuri kuliko mitandao yote.
Humo, mbali na kuchati na watu wengine, pia kulikuwa na sehemu za michezo mbalimbbali ya magari, mpira na michezo mingine, kulikuwa na saa, kulikuwa na sehemu ya kuzitumia hoteli mbalimbali oda za chakula ulichokuwa ukihitaji na kufikiwa mahali ulipokuwa ndani ya dakika chache mara baada ya kufanya malipo yako.
Kulikuwa na sehemu ya ramani iliyokuwa ikionyesha sehemu ulipokuwa. Kwa mfano mtu akitaka kutoka Massachuesetts mpaka New York, alikuwa akiangalia hapohapo na ilimpa majibu juu ya umbali, muda ambao angetumia kama angetembea, kupanda ndege au basi.
Ulikuwa mtandao mkubwa na siku hiyo ambao uliwekwa wazi, zaidi ya watu milioni ishirini waliufungua na kuangalia kilichokuwa kikiendelea. Kila mtu aliupenda, muonekano wake ukavutia na kumfanya kila mtu kutamani kuutumia siku zote.
“Ooh my God! I can’t believe,” (Ooh Mungu wangu! Siamini) alisema msichana mmoja huku akionekana kushangaa mara baada ya kuuona mtandao huo.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kabisa mtandao huo kuwekwa hewani lakini tayari kulikuwa na makampuni zaidi ya mia tano ambayo yalitaka kuweka biashara zao ziwe zinatangazwa ndani ya mtandao huo kwani uliaminika kwamba unaweza kuchukua watu wengi zaidi ya mitandao mingine ya kijamii.
Hayo yalikuwa mafanikio makubwa kwa William, hakutaka kuchelewa, akaingia mkataba na makampuni hayo na kuingiza kiasi cha dola milioni kumi kwa siku moja tu. Huo wala haukuwa mwisho, hoteli, apartments, majengo mengine, klabu za mipira, sekta mbalimbali duniani zilihitaji kutangazwa humo, hakukuwa na tatizo, wakatangazwa na kulipia kiasi kikubwa cha fedha.
“We are about to fall down,” (tunakaribia kuanguka) alisikika jamaa mmoja wa Facebook.
“We have to do something,” (inabidi tufanye kitu) alisema meneja wa mtandao huo, Bwana Sam Peters.
“What is it?” (kitu gani?)
“We must shut down the MeChat?” (ni lazima tuuzime MeChat)
“No problem, let The Man do it,” (hakuna tatizo, muache The Man afanye kazi hiyo) alisema meneja wa mtandao huo.
Kwa jina lake aliitwa Gabriel Hernandez ila kwa utaalamu wa kuchezea kompyuta ndani ya Kampuni ya Facebook, wakampa jina la The Man. Mbali na Yeye ndiye aliyekuwa mbunifu wa mkubwa wa mtandao huo, ndiye aliyekuwa akiamua leo mtandao ukae hivi au ukae vile.
Ndiye ambaye aliamua kuuendesha mtandao wa Facebook nchini China japokuwa serikali ya nchi hiyo ilikataa mtandao huo kufanya kazi nchini humo. Jamaa alikuwa mtaalamu, alijua kuichezea kompyuta, aliwahi kuizima mitandao mingi kwa maslahi yake binafsi, alikuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote na hakuna ambaye angegundua kitu chochote kile.
Huyo ndiye aliyepewa jukumu la kuuzima mtandao huo. Alipoambiwa kazi aliyotakiwa kuifanya, kwanza akaingia katika mtandao huo na kuanza kuuangalia, ulionekana kuwa mwepesi kuzimwa kuliko mitandao mingine yote. Hakukuonekana kuwa na kazi hata mara moja, kabla ya kufanya kazi hiyo, kitu cha kwanza akamuita meneja wake, Bwana Sam Peters na kumwambia kwamba angefanikiwa kufanya jambo hilo ndani ya dakika chache tu.
“Just shut it down like you did to MySpace,” (uzime kama ulivyouzima Mtandao wa MySpace) alisema Bwana Peters, hawakumwambia Mkurugenzi Zuckeberg, walitaka kufanya kwa siri kubwa, kazi ikaanza kufanyika huku The Man akiwa ameagiza soda na kuanza kunywa taratibuuuuu.
Je, nini kitaendelea?
Je, mtandao utazimwa?
Je, vipi kuhusu Warusi na mpango wao wa kumteka William?
Je, watafanikiwa?
Post a Comment