ECOWAS: Hakuna makubaliano yoyote ya Jammeh kutoshtakiwa
***
Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamesema kuwa, hakuna makubaliano yoyote ya kutoshtakiwa kwa rais Yahya Jammeh yaliyofikiwa mwishoni mwa juma, makubaliano yaliyomshawishi kiongozi huyo kuondoka mwenyewe kwa hiari nchini mwake, amesema waziri wa mambo ya Kigeni wa Senegal.
Jammeh,
ambaye anatuhumuwa kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu wakati wa
utawala wake, aliliongoza taifa la Gambia kwa miaka takriban 22, lakini
akakataa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Desemba mosi mwaka jana.
Jammeh
aliondoka mjini Banjul siku ya Jumamosi, saa chache kabla ya vikosi vya
ukanda wa ECOWAS kuingia mjini Banjul kudhibiti hali ya usalama na
kuandaa mazingira ya rais Adama Barrow kurejea.
Kuondoka
kwa Yahya Jammeh nchini Gambia kunatoa nafasi sasa kwa rais Barrow
kurejea nchini mwake baada ya kuwa amekula kiapo katika ubalozi wa nchi
yake nchini Senegal.
Uamuzi
wa Jammeh kuondoka nchini mwake, ulizua maswali kuhusu makubaliano
yaliyofikiwa kati yake na wakuu wa nchi za ECOWAS katika mazungumzo ya
siku mbili mfululizo mwishoni mwa juma, mazungumzo yaliyoongozwa na rais
wa Guinea, Alpha Conde na mwenzake wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel
Aziz.
Akizungumza
na shirika la habari la Reuters, waziri wa mambo ya kigeni wa Senegal,
Mankeur Ndiaye, amesema kuwa, wakuu wa nchi za ECOWAS hawakukubaliana
chochote kuhusu kutoshtakiwa kwa Jammeh licha ya kufikia makubaliano.
Waziri
Mankeur amesema kuwa Jammeh na timu yake walikubali kuondoka baada ya
kuahidiwa usalama na kupewa hakikisho chini ya makubaliano
yaliyopendekezwa na umoja wa Mataifa, ECOWAS na umoja wa Afrika,
makubaliano ambayo hata hivyo hayakutiwa saini na upande wowote.
Waziri
huyu amesema haya baada ya kutolewa kwa chapisho la makubaliano ya
umoja wa Afrika na umoja wa Mataifa kuhusu mapendekezo ya kufikia suluhu
ya amani ya kisiasa nchini Gambia.
Katika
hatua nyingine, vikosi vya nchi za ECOWAS tayari vimewasili mjini
Banjul, Gambia, ambako vimeenda kwaajili ya kutoa usalama kwa rais
Barrow na raia wa Gambia.
Chanzo:RFI
Chanzo:RFI
Post a Comment