Kikwete Atunukiwa Tuzo Ya Uongozi Wa Kisiasa Na Utetezi

Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete, akipokea Tuzo ya Uongozi wa Kisiasa na Utetezi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Speak Up Africa Bi Kate Campana, katika hafla iliyofanyika siku ya Alhamisi New York Marekani. Tuzo hiyo ni kutambua jitihada na juhudi zake za kufikisha huduma za jamii hususani afya kwa kwa wanawake na watoto.
...Baada ya kupokea tuzo yake.

...Akitoa hotuba baada ya kukabidhiwa tuzo ambapo alisema tuzo hiyo ni kwa watoto wote wa Afrika ambao ndiyo walimwezesha kuipata.


...Akitoa hotuba baada ya kukabidhiwa tuzo ambapo alisema tuzo hiyo ni kwa watoto wote wa Afrika ambao ndiyo walimwezesha kuipata.

Watu waliohudhuria katika hafla hiyo wakimsikiliza.
Na Mwandishi Maalum, New YorkShirika lisilo la Kiserikali la Speak Up for Africa limemtunuku tuzo, rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
Utoaji wa tuzo hiyo ya uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Speak up Africa. Hafla hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York ilikuwa pia ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji wa shughuli za taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa na Speak Up Africa, taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Kikwete, ni katika maeneo ya upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto, udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia kampeni ya Malaria Haikubaliki, usambazaji wa vyandarua vyenye viatilifu, kampeni ya lishe bora, na kampeni ya chanjo kwa watoto.
Pamoja na kutambua juhudi zake katika kuyasemea maeneo hayo, taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kulisema Bara la Afrika kila mara alipopata fursa ya kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwa ajili ya watu wenye mahitaji ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
Akipokea tuzo hiyo, amesema tuzo hiyo ni ya watoto wote Waafrika ambao ndiyo waliomfanya asimame mbele ya wageni waalikwa.
“Ni kwa sababu yenu ndiyo sababu nimetenga muda wangu baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya kuboresha maisha yenu. Ninafanya hivyo kwa sababu makuzi yangu yalikuwa kama ya mtoto yeyote yule wa Kiafrika, nimeyaishi maisha wanayoishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika hamu na kiu yao ya kuwa na maisha bora na afya njema,” akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.
Akaongeza kuwa, mafaniko ambayo ameyapata katika juhudi hizo za kufikisha huduma za msingi za kijamii kwa makundi yenye mahitaji yametokana na mambo mawili makubwa moja ni aina ya uongozi alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili uhamasishaji uliofanyika katika kupiga vita malaria kupitia Speak Up Africa na kampeni yao ya malaria haikubaliki.
“Nisingeweza kuyafanya niliyoyafanya bila uungwaji mkono na ushirikiano wa karibu nilioupata na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa ikiwamo hii ya Speak Up Africa. Ndiyo maana, kwa mfano, tumeweza kupunguza malaria kwa theluthi mbilli, tumefanikisha upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na kupunguza vifo vitokanavyo na malaria kwa nusu,” alisisitiza Kikwete na kushangiliwa tena.
Alisema anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya Hakuna Tena Malaria, Taasisi ya Billy na Melinda Gates na Gavi Vaccination Alliance ambayo anashirikiana nayo kwa karibu katika kampeni ya chanjo kwa wote.
Kikwete amewahakikishia watendaji wa Speak Up Africa kwamba ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu kutokana kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifanya.
Aliwasihi wadau mbalimbali kuichangia taasisi hiyo kwa kile alichosema, inafanya kazi kubwa na siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa lakini pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.
Wengine waliopewa tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni pamoja na Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya wa Senegal, Bibi Toyin Saraki, mwanzilishi wa Taasisi ya Wellbeing Afrika ambayo pia imekuwa ikitoa elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua. Pia alikuwemo Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wari.
Taasisi ya Speak Up Africa imeanzishwa na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uwezo na sifa kubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.
Post a Comment