Dk. Magufuli Amtumia Salamu Za Rambirambi Mkuu Wa Mkoa Wa Tanga Kufuatia Ajali Vifo Vya Watu 11
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemtumia salamu za rambirambi Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Bi. Mwantumu Mahiza, kufuatia vifo vya watu 11
waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyosababishwa na Basi la
Kampuni ya Simbamtoto kugongana uso kwa uso na Lori lililobeba mchanga
katika eneo la Pandamlima, Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga.
Ajali
hiyo imetokeo leo tarehe 11 Februari, 2016 majira ya saa 1:15 asubuhi
katika eneo hilo lenye mteremko, ambapo basi la Kampuni ya Simbamtoto
lilikuwa likisafiri kutoka Tanga kwenda Dar es salaam na Lori lililokuwa
limebeba mchanga, lilikuwa likielekea kiwanda cha saruji cha Tanga.
Rais
Magufuli amewapa pole Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliofikwa na msiba
huo na amewataka kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika kipindi hiki
kigumu.
"Nimepokea
taarifa ya vifo hivi kwa mshituko mkubwa, na kupitia kwako Mkuu wa Mkoa
wa Tanga, napenda kuwapa pole nyingi wote waliofikwa na msiba huu
mkubwa na naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo" alisema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema pepo, na
amewapa pole majeruhi wote 21 walioumia katika ajali hii.
Aidha,
Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wote wa barabara hususani
madereva wa vyombo vya moto, kuwa makini watumiapo barabara kwa
kuzingatia sheria zote zinazosimamia usalama barabarani ili kuepusha
ajali.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam.
11 Februari, 2016
Post a Comment