ad

ad

KAKA NAPE KWENYE MICHEZO HUHITAJI KUSHITUKIZA, WAPE TAARIFA HALAFU NENDA UKAKUTANE NA MADUDU

 Na Saleh Ally
KIU ya Watanzania wengi kulijua baraza la mawaziri la serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli iliisha jana.


Serikali ya Magufuli imekuwa ikifanya kazi ikiwa na viongozi wachache tu, lakini imechachafya ile mbaya kwa kipindi cha mwezi mmoja na mabadiliko yameonekana.

Tumeona namna vigogo kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), bandari na kwingineko walivyokumbwa na mafuriko ya Rais Magufuli na serikali bado haikuwa na baraza la mawaziri.

Wakati wa kampeni zake, Rais Magufuli aliahidi kuunda baraza dogo la mawaziri. Kweli ametangaza mawaziri 30 tu, huku akiahidi kumalizia kuwatangaza wengine wanne hapo baadaye.
Katika baraza hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameteuliwa Nape Nnauye kushika wadhifa huo na sasa wanamichezo watakuwa wamekata kiu yao ya kujua nani atakuwa kiongozi au mwakilishi wao hasa serikalini.

Nape amekuwa akikitumikia cheo cha Katibu Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), lakini sasa ni kwa ajili ya Watanzania wote na kikubwa ni kuendeleza kinachotakiwa kupitia wizara yake.

CCM ni kubwa, kuna mambo mengi yanayohusu vijana halikadhalika michezo na Nape hatakuwa mgeni. Ndani yake kuna masuala ya wasanii ambao pia wamekuwa wakihusishwa na mambo mbalimbali ya chama hicho kikubwa. Pia kwa kuwa waziri huyo ni kijana kabisa, hakika kuna uwezekano wa kupatikana mabadiliko makubwa.

Wakati Rais Magufuli alipoingia madarakani, alianza na staili ya kuvamia sehemu kadhaa bila ya taarifa na kweli amekumbana na madudu kibao ambayo tayari yameanza kushughulikiwa.

Katika michezo kuna mambo mengi sana kama kweli ambayo yanahitaji mtu asiyetaka mchezo ili kurudisha nidhamu na kuwafanya watu wa michezo sasa waamini nidhamu na kujituma ndiyo kitu sahihi katika endelezaji wa mambo.

Inawezekana katika michezo ukianzia soka, riadha, netiboli, ngumi za ridhaa na kulipwa ndiyo kuna sehemu nyingi sana za kuvamia na kuleta mabadiliko.

Kama Waziri Nape atapata sehemu ya kuvamia sehemu kibao atagundua kuna madudu mengi kupindukia na watu wamekuwa wakiitumia michezo kuvimbisha matumbo na kung’arisha nafsi zao.

Watu wengi walio katika michezo kamwe hawaijali na kwa makusudi wala hawataki kupima uwezo wao wa kiungozi badala yake wanatumia udhaifu wa wanamichezo wengi kuwalaghai na hata kuwapa rushwa wawachague.

Kuna ile methali isemayo hivi: “Akili haba na madaraka makubwa ni msiba”. Hakika katika michezo tuna misiba lukuki, watu wengi hawajiwezi kiutendaji, lakini kwa umahiri wao wa ushabiki, ushawishi mkubwa wa midomo au fedha zao unawapa nafasi ya kuendelea kuwa viongozi wa juu lakini wasio na msaada wowote katika uletaji maendeleo zaidi ya kutuachia msiba.

Ninajua kabisa kuwa “vita vya bunduki haviamuliwi kwa fimbo”. Lakini namkumbusha Waziri Nape kwamba “vya zamani si vya leo” na lazima akaze kamba ili watu waondokane na yale mambo ya kuamini kila kitu kilikuwa kinakwenda kwa mazoea.

Watu wamejimilikisha taasisi za umma au mali za Watanzania katika michezo na wamejisahau kabisa kama ni za umma. Hawataki kukosolewa licha ya kwamba wana uwezo mdogo na wanalijua hilo.

Kusiwe na watu wanaotaka kusema wanaingiliwa kama wakikosolewa. Tafadhali pita kote uone michezo inavyotumika kuwafaidisha wajanja wachache huku wanaoumia wakiwa zaidi ya asilimia 90. Achana na ile ya Rais Magufuli ya kuvamia, katika michezo hata ukitoa taarifa, kila utakapokwenda hakuna mwenye uwezo wa kuyafunika maovu na uzembe wa makusudi unaofanyika kwa mikono yake. Lazima madudu hayo yataonekana tu.
Powered by Blogger.