Barua nzito: Bongo movies, twendeni na kasi ya Magufuli!

KWENU mastaa wa Bongo Movies.
Sina haja ya kuwataja majina maana najua nikifanya hivyo, naweza
nikajaza ukurasa huu. Lakini nawasalimu wote katika jina la Bwana!
Poleni na mihangaiko ya kila siku.
Poleni na mihangaiko ya kila siku.
Mimi ni mzima wa afya, namshukuru Mungu
naendelea na mapambano katika eneo langu kuendana na kasi ya rais wetu,
Dk. John Pombe Joseph Magufuli na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.
Nimewakumbuka leo kwa barua maana najua
wengi wenu hatujaonana hivi karibuni. Ni vyema pia mkasoma kile ambacho
ninacho rohoni na mkakifanyia kazi. Najua mnajua lakini si vibaya
nikawakumbusha ili kuweka msisitizo.
Dhumuni la kuwaandikia barua hii ni
kutaka kuwaambia kwamba, mnapaswa kujiandaa na ujio wa Dk. Magufuli
katika tasnia yenu. Kasi aliyoanza nayo, ni dhahiri kwamba atawafikia
muda si mrefu.
Kwa muda mrefu mlikuwa mkilia na
changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kazi zenu. Mlikuwa
mkisumbuliwa sana na wanyonyaji wa kazi zenu. Wasambazaji wachache
walikuwa wakiwapangia bei wanazotaka kununua filamu zenu, tena hati
miliki zinakuwa za kwao.
Msanii anaigiza yeye, hati miliki
inakuwa ya ‘mdosi’. Anauza anakotaka bila kuwa na mipaka. Wezi wa
kudurufu kazi zenu ni tatizo sugu. Mikataba ilikuwa haikidhi matakwa ya
msanii kiasi ambacho hakuna aliyekuwa anainjoi maisha ya uigizaji kama
walivyo wasanii wa Nigeria, Ghana na kwingineko.
Lakini ninapowaambia mjiandae,
namaanisha nyinyi wenyewe pia muamke na muanze kujiandaa na kasi ya
maendeleo. Baadhi yenu mlikuwa hamjitambui. Mlikuwa hamna misimamo
katika maamuzi yanayohusu kazi zenu.
Ndiyo maana kulikuwa na baadhi yenu
walikuwa wanapata kipato chenye nafuu lakini wengine wengi wakiwa na
hali mbaya kupindukia. Si muda tena wa kuendeleza majungu, usaliti na
vitu kadha wa kadha vinavyofanana na hivyo.
Mnapaswa kuipokea kasi ya Magufuli kwa
kuendana na mfumo atakaouweka kusimamia mapato yenu. Mnapaswa kuungana
na kupeleka mapendekezo yenu katika ofisi yake. Afanye nini ili muweze
kudhibiti wizi wa kazi zenu.
Afanye nini ili muwe mnalipa kodi halali
na stahiki huku mkinufaika kwa kipato kizuri. Muwe mnamiliki kazi zenu.
Muwe na nyenzo nzuri za kufanyia kazi zenu ili angalau muweze
kuzisogelea levo za kimataifa. Amkeni sasa, mnapaswa na nyinyi kuishi
kwa kutegemea sanaa.
Muwe matajiri wakubwa kama wasanii
wenzenu ambao tunawasoma kila siku kwenye vyombo vya habari ndiyo wenye
fedha kuliko hata viongozi wa nchi na wafanyabiashara. Sanaa inalipa
kama tu mtaamua kuifanya ‘serious’.
Rais wetu ameonesha mwanga wa
kushughulika na mafisadi, rushwa na tunaamini mambo yatakuwa sawa hivyo
msimuangushe. Nendeni na kasi yake ili muweze kupiga hatua ya kweli na
wakati sekta nyingine zitakapokuwa zinashangilia ushindi wa kasi ya
Magufuli na nyinyi pia muweze kufanya hivyo katika eneo lenu.
Ni matumaini yangu Mungu atawaongoza na mtapiga hatua, kila la kheri. Mimi ni ndugu yenu;
………………………….
Erick Evarist
Erick Evarist
Post a Comment