ad

ad

Wambura ni nouma!


HAKIKA Michael Richard Wambura ni noma, hiyo ni baada ya wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuumiza vichwa kupata muafaka juu ya suala lale la kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais katika Klabu ya Simba.

Mgombea huyo alienguliwa katika uchaguzi huo na Kamati ya Uchaguzi ya Simba iliyo chini ya mwanasheria Dk Damas Ndumbaro kutokana na kudaiwa siyo mwanachama wa klabu hiyo baada ya kufutwa kufuatia kuipeleka Simba mahakamani Mei 5, 2010.

Tangu juzi Jumatatu hadi jana, mjadala baina ya wajumbe wa kamati ya rufani kwenye Hoteli ya Courtyard, Upanga jijini Dar, ulikuwa mkubwa, lakini taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo ni kuwa Wambura amerejeshwa kwenye mchakato.

Hoja zilikuwa nzito kwa wajumbe hao na kulazimika kuchukua muda mrefu kutafuta hatima ya Wambura.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati hiyo ya rufani, Wambura amepitishwa kwa kura za wajumbe watano waliokutana kusikiliza rufaa hiyo, kura tatu zimempitisha kugombea nafasi hiyo huku mbili zikimuengua.

“Wambura tumemrudisha kwenye uchaguzi baada ya kamati ya rufani kuamua kumpitisha kugombea nafasi yake, hiyo ni baada ya kamati kukutana kupitia pingamizi alizokatiwa.

“Amepita baada ya kujadiliana kwa kina na kuona hoja alizowekewa siyo za msingi, baadaye wajumbe walichukua maamuzi ya kupiga kura ambazo zilimrejesha katika kichang’anyiro hicho. Alishinda kura tatu kati ya tano tulizopiga,” kilisema chanzo hicho.

Alipoulizwa Wambura jana jioni kuhusiana na taarifa hizo huku akionekana ni mwenye furaha, alisema: “Hadi hivi sasa sina taarifa rasmi kutoka kwenye kamati.

“Watu wengi wamekuwa wakinipigia kuniuliza juu ya taarifa hizo.”

Mjumbe wa Friends of Simba, Azim Dewji, alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo, aliitupia lawama TFF ambayo inaongozwa na Rais Jamal Malinzi.

“Ni sawa baada ya kuona TFF wanamrejesha, lakini wanachama ndiyo watakaoamua, lakini jambo la kushangaza haohao TFF walimsimamisha kwenye chaguzi mbalimbali mara sita ukiwemo wa nyumbani kwao Mara.

“Inavyoonekana TFF wana malengo ya kuivuruga Simba, hivyo sisi tunawaachia wenyewe waamue,” alisema Dewji.

No comments

Powered by Blogger.