ad

ad

Serikali, Bunge wakabana koo

Dodoma na Dar es Salaam. 
Kumekuwa na mvutano mkubwa katika vikao vya mashauriano kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambao pamoja na mambo mengine unaelezwa kuchangiwa na hatua ya Serikali kukataa kuweka wazi vyanzo vya mapato kwa wajumbe wa kamati hiyo.

Kutokana na hali hiyo, majadiliano kuhusu mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, yamejikita katika makadirio ya matumizi pekee ambayo ni Sh19 trilioni, bila kufafanua fedha hizo zinatarajiwa kutoka katika vyanzo vipi.

Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema mvutano baina ya timu ya Serikali inayoongozwa na Waziri wa Fedha, Saada Nkuya Salum kwa upande mmoja na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ni dhahiri hakuna makubaliano ambayo yamefikiwa hadi sasa.

Wajumbe wa kamati hiyo wamekuwa wakitaka kufahamu vyanzo vya mapato ili kujiridhisha iwapo Serikali imezingatia ushauri wa Bunge kuhusu kuongeza vyanzo vipya, badala ya kuongeza kodi katika vyanzo vilevile kila mwaka.


“Tunashangazwa na makadirio ya matumizi ya Sh19 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha wakati wameshindwa (Serikali) kukusanya Sh18 trilioni na kusababisha upungufu wa fedha katika bajeti ya sasa. Wakijitahidi watamaliza mwaka huu wa fedha (Juni 30), wakiwa na upungufu wa zaidi ya Sh600 bilioni, sasa tunataka kujua ni vyanzo gani vitatumika kupata hizo trilioni 19?”


Chanzo kingine kilisema madai ya wabunge kutaka kufahamu vyanzo vya mapato yanatokana na kupewa taarifa za siri kwamba Serikali inakusudia kuongeza kodi katika vyanzo vilevile vya miaka yote, vikiwamo sigara, mafuta, soda na bia, hali ambayo walihisi kuwa ni kupigwa teke kwa mapendekezo waliyoyatoa mwanzoni mwa mwaka jana.


Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alipoulizwa sababu za Serikali kuficha vyanzo vyake kwa wabunge kupitia ujumbe mfupi wa maandishi ya simu alijibu: “Nashauri swali hilo lielekezwe kwenye chanzo chako kwa kuwa mimi sina taarifa hizo.”

Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alisema taarifa zilizopo ni kwamba Kamati ya Bajeti na Serikali walikuwa wakiendelea na majadiliano na kwamba vikao husika vitaendelea leo... “Hakuna taarifa zozote rasmi kutoka ndani ya kikao hicho, tusubiri maana Alhamisi siyo mbali tutafahamu tu, tuwe na subira.”


Kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Bajeti, Chenge aliongoza Kamati Maalumu iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kuchunguza mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Iliwasilisha taarifa iliyobaini madudu katika mfumo wa bajeti.

Katika ripoti yake, kamati hiyo ilibainisha kuwapo kwa udhaifu katika ukusanyaji wa mapato na kwamba kwa mwaka wa fedha 2012/13 pekee, Serikali ilipoteza Sh3.95 trilioni kutokana na kasoro zilizopo.

Mapendekezo ya Bunge


Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Spika Makinda Februari 8, mwaka jana na baadaye kuwasilishwa serikalini, ina mapendekezo ya vyanzo vipya 24 vya mapato ambayo Chenge alisema kama yangetekelezwa yangeiwezesha Serikali kupata ziada ya Sh14.86 trilioni katika bajeti zake za 2014/15 na 2015/16.
Vyanzo hivyo ni pamoja na uvuvi katika eneo la Bahari Kuu ambalo lilitajwa kuwa moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakiikosesha Serikali mabilioni ya shilingi kutokana na meli za kigeni kuvua kiholela bila kukaguliwa.


Uchambuzi wa kamati hiyo ambayo wajumbe wake wengi ndiyo wanaounda Kamati ya Bajeti, ulionyesha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya 1998 ni kikwazo cha upatikanaji wa kiasi cha Sh352 bilioni kila mwaka kutokana na kutokuwa na kifungu cha kutoza mrabaha.

Pia ilitaja miradi ya gesi kwamba baada ya yote kukamilika, likiwamo bomba la Mtwara hadi Dar es Salaam, inaweza kuliingizia taifa Sh716.61 bilioni kwa miaka mitatu kuanzia 2015 – 2017.

“Kwa mfano, kiasi kilichogundulika ni futi za ujazo trilioni 32 ambazo ni sawa na mapipa bilioni 6 ya mafuta. Kwa bei ya sasa gesi hii ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 660,” alisema Chenge.

Alisema iwapo mgawo wa Serikali ni angalau asilimia 10 na ikaamua kuutumia kama dhamana au mauzo ya mbele (collateral or forward sale), itapata Dola za Marekani bilioni 6.6, sawa na Sh10.56 trilioni ambazo zinaweza kutumika katika bajeti za 2014/2015 na 2015/2016.

Kamati hiyo pia ilibaini kwamba iwapo Serikali ingetimiza ahadi yake ya kuliwezesha Shirika la Petroli Tanzania (TPDC), kutumia fursa ya uwekezaji kwa asilimia 20 katika mkataba wa utafutaji wa mafuta wa Mnazibay zinaweza kupatikana Sh33.8 bilioni kwa mwaka.

Makaa ya mawe yalitajwa kuwa yanaweza kusaidia kuokoa kiasi cha Sh1.1 trilioni kwa mwaka, kiasi ambacho kinatumiwa sasa na Serikali kwa ajili ya kugharamia mafuta ya kuzalisha umeme.

Ilishauriwa kuwa Serikali inapaswa kufanya uamuzi kutumia gesi kama chanzo cha mapato kwa kuweka dhamana kiasi kidogo cha gesi.

Walipendekeza kuanzishwa kwa tozo mpya katika huduma za usafirishaji wa fedha kupitia simu za mkononi, hivyo kuiwezesha nchi kuingiza Sh25.5 bilioni kwa mwaka na uanzishwaji wa ada ya utumiaji wa kadi za simu za mkononi yenye uwezo wa kuingiza Sh255.5 bilioni kwa mwaka.

Kauli ya Serikali

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema katika bajeti ijayo, Serikali itachukua hatua za kuongeza mapato yake ili kukwepa upungufu wa fedha uliojitokeza katika bajeti ya 2013/14 na kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Tutakuja na mapendekezo ya jinsi ya kukusanya mapato ya ndani, maana kujitegemea kuna heshima yake na kunachochea maendeleo. Tutakuja na mapendekezo hayo na tunaomba wananchi na wabunge watuunge mkono” alisema Nchemba.

Alisema hatua nyingine ni kuimarisha usimamizi wa fedha zinazopatikana licha ya kuwa ni kidogo. “Tutakavyotengeneza Sheria ya Bajeti, lengo lake ni kuimarisha usimamizi wa fedha zote zinazotumika ili kuleta thamani ya fedha iliyokusudiwa” alisema Nchemba.

Alisema jambo lingine ni kuhakikisha fedha ambazo hazitokani na kodi zinatumika kutekeleza miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo.

“Wananchi wanaweza kuchanga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule, jengo linapokamilika wahandisi hujitokeza na kudai kuwa limejengwa chini ya kiwango. Katika eneo hili kuna upotevu mkubwa wa fedha ambao tutaudhibiti,” alisema.

Nchemba aligusia suala la ukwepaji wa kodi na kusema nchi imekuwa ikiwategemea wafanyabiashara wadogo na wafanyakazi pekee na kusema watakuja na njia nyingine ya kuongeza vyanzo vya mapato.

“Tunalenga kupunguza kodi kwa wafanyakazi ili kuwapunguzia gharama za maisha ambazo zinapanda kila siku. Pia tutaziba mianya ya ukwepaji wa kodi,” alisema.

Nyongeza na Fidelis Butahe na Sharon Sauwa (Dodoma)
 CREDIT: MWANANCHI GAZETI LA LEO

No comments

Powered by Blogger.