ad

ad

AZAM BINGWA LIGI KUU


Na Martha Mboma, Mbeya
ILIKUWA kama vita lakini hatimaye mechi imefanyika, matokeo yamepatikana na rekodi imewekwa kwenye ardhi ya Mbeya, Azam FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, jana.
Azam ambayo imefikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo, imeweka rekodi nyingi kutokana na ushindi huo, lakini habari mbaya ni kuwa mashabiki na wachezaji wa Mbeya City walijikuta wakimwaga machozi, huku mwamuzi wa mchezo huo, Nathan Lazaro akitoka uwanjani akiwa chini ya ulinzi mkali.

Rekodi zilizowekwa
Azam imekuwa timu ya kwanza mbali ya Simba na Yanga, kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2,000 Mtibwa Sugar ilipobeba ubingwa huo, pia ni timu ya kwanza kubeba ubingwa kwa timu ya Dar es Salaam mbali ya vigogo hao ambao wamekuwa wababe wa ligi hiyo kwa miaka mingi.
Azam imekuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye uwanja wake wa nyumbani msimu huu, pia imeweka rekodi ya kutwaa ubingwa bila kupoteza mechi hata moja kama ambavyo Simba ilifanya miaka kadhaa iliyopita wakati ilipokuwa ikinolewa na Mzambia Patrick Phiri.

Mwamuzi awavuruga Mbeya
Mpaka dakika 45 zinakamilika, Azam ilikuwa ikiongoza kwa bao moja lililofungwa na Gaudence Mwaikimba dakika ya 45, kuona hivyo wachezaji wa Mbeya City walianza kulaumiana huku mashabiki wakisikika wakisema: “Ole wenu mfungwe, hamtoki humu leo.”
Kauli hiyo ni kama iliwafikia wachezaji kwani waliongeza kasi na kusawazisha bao katika dakika ya 70 kupitia kwa Mwegane Yeya. Mechi ikawa ya kukamiana huku mwamuzi akionekana kupata wakati mgumu kutoa maamuzi kutokana na vurugu za hapa na pale za wachezaji wa timu zote.
Bao la pili lililofungwa na John Bocco dakika ya 85, lililotokana na beki wa Mbeya City, Antony Matogolo kuanguka wakati akiwania mpira na Mwaikimba kisha Bocco akauchukua na kutupia wavuni, hapo ndipo wachezaji wa Mbeya City wakamvaa mwamuzi na kuhoji sababu za kuruhusu bao wakati wanaamini mchezaji wao alifanyiwa madhambi.
Mzozo huo ulisababisha Paul Nonga kupewa kadi nyekundu huku mashabiki wao nao wakilalama kuonewa.
Baada ya mechi hiyo ilibidi askari kuzunguka uwanjani na kuwalinda mwamuzi na washika vibendera kutokana na wachezaji wa Mbeya City na mashabiki wao kuonekana kukasirishwa na maamuzi yake.

Ulinzi & vilio
Mashabiki kadhaa wa Mbeya City walianza kulia na wengine kugaragara kwenye matope wakilalama mwamuzi kuwamaliza, huku wachezaji wa Mbeya City nao wakimwaga machozi.
Mashabiki hao waligoma kutoka uwanjani huku waamuzi wakisindikizwa kutoka chini ya ulinzi mkali, baada ya muda askari walianza kumwaga maji ya kuwasha kwa mashabiki waliokuwa wamegoma kutoka uwanjani, lakini dakika chache baadaye wote walitoka na uwanja ukabaki mweupe.
Akizungumzia mchezo huo uliochezwa huku mvua ikinyesha, Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala alisema: “Mwamuzi anatakiwa kujilaumu mwenyewe kwa kuwa alishindwa kuumudu mchezo kwa kuruhusu matukio ambayo hayakuwa ya kiuanamichezo.”
Upande wa benchi la ufundi la Mbeya City, hakuna aliyezungumza, wote waliondoka bila kutaka kuelezea chochote.

No comments

Powered by Blogger.