YANGA, AZAM ZAGONGANA KWA AMISSI TAMBWE
NYOTA ya mshambuliaji hatari wa Simba, Amissi Tambwe inazidi kung’aa baada ya timu mbili zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Yanga na Azam, kuulizia huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.
Tambwe, raia wa Burundi, amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu tangu atue Simba akitokea Vital ‘O ya Burundi ambapo kasi yake ya kufunga mabao ndiyo chanzo kikubwa cha miamba hiyo ya soka nchini kumnyemelea, akiwa amefunga mabao 19 katika ligi kuu.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo ambaye ndiye amekuwa mshauri mkuu wa Tambwe, alisema kuwa Yanga na Azam FC wamevutiwa na kiwango cha straika huyo na tayari wameanza kufanya mchakato wa kumsajili kwa kuwa wanaona Simba haina matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
Habari kamili ni kuwa tayari mazungumzo ya usajili yameanza kupitia wakala wa mchezaji huyo ambaye alimleta nchini kutoka Burundi.
Mtu huyo amesema pamoja na michakato hiyo, bado Yanga na Azam hazijafanya mawasiliano ya moja kwa moja na Tambwe kwa kuwa bado ana mkataba na Simba.
“Yanga na Azam zote zinamtaka Tambwe kwa ajili ya msimu ujao, ile spidi yake ya kufunga ndiyo wengi wamevutiwa nayo, lakini tayari juhudi kwa ajili ya kumnasa zimeshaanza kufanyika.
“Katika siku chache zilizopita, watu kutoka Azam na Yanga walimtafuta yule wakala wake aliyemleta Simba, wakazungumza naye kwamba wanamtaka jamaa atue kwao na ikiwezekana msimu ujao awe tayari ameshaanza kazi,” alisema rafiki huyo na kuongeza:
“Ila tayari hizi taarifa mwenyewe Tambwe zimeshamfikia, anafahamu kwamba anahitajika na timu nyingine msimu ujao, kuna watu wake wa karibu walimtonya na kumuelezea kila kitu.”
Gazeti hilolilipowasiliana na Tambwe juu ya suala hilo, alisema: “Ni timu nyingi tu nimeambiwa zinanihitaji lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote kuhusu hilo, bado nipo chini ya Simba, kama kuna lolote uongozi wangu upo, nafikiri huko ndiko kunaweza kukawa na mzungumzo juu yangu kwa sasa.”
Wakati huohuo, Tambwe amesema atarejea kwenye mazoezi Jumatatu. “Wiki hii napumzika kabisa, Jumatatu ndiyo nitaanza mazoezi rasmi, kidonda kimeshaanza kukauka,” alisema Tambwe.
CHANZO NI CHAMPIONI IJUMAA
Post a Comment